MAKALI YA RONALDO EURO

Advertisements

Kadri michuano hii ya EURO 2020 inavyoendelea, ndivyo ladha yake inazidi kunoga na kukolea eti. Imekuwa asali ikoleayo magegoni. Katika makala ya jana nilisema kuwa kila mechi ni kubwa na ewaaa, msomaji huna budi kukubali kuwa yalidhihirika wazi. Wengi walikuwa wanatazamia mechi ya Ufaransa dhidi ya Ujerumani lakini kabla ya kufika kule mbona tusizungumzie Ureno na Hungary?

Advertisements

Hiyo jana mechi ya ufunguzi wa kundi ‘F’ ilishirikisha Ureno na Hungary, mechi ambayo kwamba ilikamilika kulingana na matarajio ya wengi. Ila tu kwa kipindi fulani mechi hiyo ilitamausha na naridhia kwamba ningekuwa mmoja wa wale ambao hubashiri mbashara huenda ningecheza na sare. Tena sare tasa lakini lo! Ndio mwanzo wengi walifahamu hapo jana kuwa mchezo wa soka ni dakika tisini. Mahasidi wa Ureno na mashabiki wa Hungary walikuwa washakata kanzu kabla hawajamwona mwana. Tayari walikuwa washaanza kuhesabu vifaranga kabla hata kuku mwenyewe hajataga. Yaani tayari walikuwa washajichukulia alama moja ya sare dhidi ya bingwa mtetezi! Mambo yangesalia vile huenda makala ya leo yangehusu tope kukataa mfinyanzi lakini ghafla Raphael Guerriro mnamo dakika ya 84 ya mchezo akazamisha mawazo yao. Christiano Ronaldo naye akadhihirisha waziwazi ni kwa nini ana tuzo tano za Ballon dior kwa kufunga magoli mengine mawili katika dakika za 87 na 92 mtawalia. Na hiyo ikawa mechi ya kuandikisha historia kwake. Ronaldo kwa sasa ndiye mchezaji pekee kuwahi tokea kwenye fainali tano mtawalia na pia ndiye mfungaji bora katika historia ya kombe hili la EURO akiwa na mabao 11. Katika kampeni za mwaka huu au msimu huu Ronaldo tayari yuko miongoni mwa wafungaji bora kufikia sasa.

Wafungaji bora EURO kufikia sasa

Ufaransa nao walionyesha mchezo mzuri hasa sana Paul Labile Pogba akionyesha jinsi anavyoweza kuwa mbunifu na kutamalaki kwenye safu ya kati. Wafaransa waliwahemesha wajerumani na kuwageuza mambumbumbu na mazuge wasiojua soka hadi ya kujifunga bao. Bao hili la kujifunga ndilo liliwaponza kushindwa mechi ile. Kundi hilo kwa sasa linaongozwa na Ureno ikifuatiwa kwa karibu sana na Ufaransa tofauti ikiwa mabao mawili baina yao kisha Ujerumani na Hungary mtawalia wote wakijivunia alama sufuri.

Msimamo wa kundi F kufikia sasa

Leo hii ni mechi za mzunguko wa pili kundi A. Hapo saa kumi juu ya alama Finland watakipiga na Urusi, Uturuki na watamkaribisha Wales saa moja kamili na hapo baadae mida ya saa nne usiku Italia watatumbuiza na Uswizi. Saa zote ni majira ya Afrika ya Mashariki. Ikumbukwe kuwa Italia ndio wanaoongoza kundi hilo. Je, tuwekeze wapi?

Ratiba ya mechi za leo
  • #TwendeEuroNaUnityMedia254
Advertisements

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *