TWENDE EURO

Advertisements

Ni raha iliyoje kwa wapenzi kindakindaki wa kandanda kote ulimwenguni shirikisho la soka bara ulaya (UEFA) kwa mara nyingine tena inapoleta kombe la EURO. Ni furaha bila shaka pia kwa wawekezaji na wabashiri ila kufikia sasa mechi hizi zinapoendelea katika hatua za makundi utakubaliana nami kuwa hakutabiriki kamwe. Hebu chukua mfano wa mechi ya jana ya kundi E ambapo Uhispania na Uswizi walivuna sare tasa, Alvaro Morata akikosa nafasi ya wazi na kujigeuza ‘Mohata’. Nao Scotland walikubali kushindwa mawili kavu na Jamhuri ya Czech. Ama kweli mpira hudunda!

Advertisements

Michuano hii kwa kweli ilianza kwa pupa, papara na joto jingi ili tu kuleta ladha na kuzidisha ilhamu kwa mashabiki na maashiki wa mchezo wa soka, japo kwa makundi mengine hali ni ile ya vitu vizuri havitaki haraka. Katika mechi ya ufunguzi Italia waliwalabua Uturuki bila ya kumtazama mabao matatu bila jibu huku Romelu Lukaku akihakikisha Ubelgiji inaongoza jedwali la kundi B kwa kumzamisha Mrusi magoli matatu bila jawabu.

Jedwali la kundi B kufikia sasa

Kwingineko ni vijana wa Malkia, Uingereza, almaarufu ‘The three Lions’ walijiwekea rekodi mpya ya kushinda mechi ya ya ufunguzi kwa mara ya kwanza katika historia ya michuano hii ya EURO. Hii ni baada ya Raheem Sterling kufunga bao la pekee na la ushindi dhidi ya Croatia. Uingereza pia waliweka rekodi nyingine ya kumchezesha mchezaji kinda sana katika michuano ya EURO. Hii ni baada ya mkufunzi wa The Three Lions, Gareth Southgate, kumleta Jude Bellingham kuchukua nafasi yake nahodha Harry Kane katika mechi iyo hiyo ya Uingereza na Croatia.

Katika fungua fungua za michuano hii, kulishuhudiwa jambo la kusikitisha na kutamausha kwa taifa la Denmark na Dunia nzima kwa upana baada ya Christian Eriksen kuzimia uwanjani dakika chache tu baada ya mechi ya Denmark na Finland kung’oa nanga. Shukran kwa nahodha wa Denmark Simon Kjaer kwa kumpa huduma ya kwanza gwiji huyo wa safu ya kati, vinginevyo ingekuwa makala tofauti hapa mpenzi msomaji. Shirikisho la soka bara Ulaya walimtunuku Eriksen nyota wa mechi hata baada ya Finland kuwafinya Denmark moja bila. Ikumbukwe mechi hiyo iliahirishwa sababu ya tukio hilo na kurejelewa baadae.

Kila mechi ni kubwa. Hebu tuzungumzie mechi za leo ambapo Hungary na Ureno watakutana saa kumi na mbili jioni saa za Afrika Mashariki nao fahali Ufaransa na Ujerumani wakiumiza nyasi saa nne juu ya alama majira ya usiku saa za Afrika Mashariki.

Ratiba ya michuano ya EURO leo hii

Je itakuwa Mbappe ama Werner. Zidi kutegea Unity Daily News halikadhalika Unity Radio 254 kwa takwimu, uchambuzi, uchanganuzi na habari zote za EURO 2020 kwani hapa ndipo na sisi ndisi.

#TwendeEuroNaUnityMedia254.

Advertisements

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *